31/08/2026
JAMII YAKUMBUSHWA UMUHIMU WA KUTUNZA AFYA YA UBONGO, UTI WA MGONGO NA MISHIPA YA FAHAMU
Jamii imetakiwa kuchukua hatua za kulinda afya ya ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, kutokana na umuhimu wa viungo hivyo katika uwezo wa mtu kufikiri, kutembea, kuzungumza na kufanya shughuli mbalimbali za kila siku.
Rai hiyo imetolewa na Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dkt. Kigocha Okeng’o, ambaye amesema utunzaji wa mfumo wa fahamu ni muhimu kwa afya na ustawi wa mtu kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Dkt. Okeng’o ulaji wa lishe bora, kufanya mazoezi mara kwa mara, kupata usingizi wa kutosha pamoja na kudhibiti magonjwa k**a shinikizo la damu na kisukari, ni miongoni mwa hatua zinazoweza kusaidia kulinda afya ya ubongo na mfumo wa fahamu.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuzuia majeraha ya kichwa na uti wa mgongo kwa kuzingatia kanuni za usalama barabarani, ikiwemo matumizi sahihi ya helmeti kwa waendesha pikipiki na baiskeli, pamoja na mikanda ya usalama kwa watumiaji wa magari.
Ameeleza kuwa, jamii inapaswa pia kuzingatia usalama katika maeneo ya kazi na wakati wa kufanya shughuli mbalimbali ili kupunguza uwezekano wa kupata majeraha yanayoweza kuathiri ubongo, uti wa mgongo au mishipa ya fahamu.
Aidha, amewataka wananchi kutopuuza dalili za hatari zinazoweza kuashiria tatizo katika mfumo wa fahamu, zikiwemo ganzi, udhaifu wa mwili, matatizo ya kuzungumza au kuona, kupoteza usawa pamoja na maumivu makali ya kichwa yanayoanza ghafla.
Amesema kutafuta huduma ya afya mapema mara tu dalili hizo zinapotokea ni muhimu katika kusaidia kutambua tatizo na kuanza matibabu kwa wakati. Muhimbili Taifa Wizara Ya Afya Elimu Ya Afya Kwa Umma