12/05/2026
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe, Bi. Kuruthum Sadick ametoa wito kwa wauguzi wote Hlamashauri ya Mji wa Njombe kutanguliza utu na huduma bora kwa wananchi ili kutimiliza sifa ya wito kwa kada hiyo.
Ametoa kauli hiyo katika kilele cha Maadhimisho ya wiki ya Wauguzi duniani leo Mei 12, 2026, ambayo imefanyika katika viwanja vya Stendi ya zamani ya Halmashauri ya Mji Njombe.
Bi. Kuruthum amesema kuwa Uwekezaji katika vifaa na ongezeko la Ajira za Uuguzi uliofanywa na serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umechagiza kwa kiasi kikubwa kupunguza simu za Malalamiko ya wananchi na hivyo akatoa wito kwa watumishi wa kada hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi hizo za Mhe. Rais.
Naye Mganga Mkuu, Halmashauri ya Mji Njombe, Dkt. Jabil Juma, amesema ipo haja kubwa ya wauguzi kuelewa kuwa waajiri wao ni wananchi, hivyo kuenenda kinyume na utumishi wao inaweza kuzorotesha Afya ya wananchi, ulemavu wa kudumu hadi kifo; kwa kauli hiyo akawataka kuendelea kutoa huduma za kuridhisha ili kuendelea kuwahamasisha wananchi kurudi na kupata huduma katika vituo vyao vya kutolea huduma.
Maandamano ya Amani ya Siku ya Wauguzi Duniani katika Halmashauri ya Mji Njombe, yalitanguliwa na kuwatembelea wagonjwa waliolazwa katika kituo cha Afya cha Kanisa la Anglican kilichopo, Chaugingi, Halmashauri ya Mji Njombe, kisha baadae kuelekea Viwanja vya Stendi ya Zamani, ambapo zilifanyika shughuli mbalimbali, ikiwemo Sanaa ya Maigizo yenye lengo la kutoa ujumbe kwa jamii kuhusu huduma za Uuguzi.